Saturday, January 31, 2015

Elimu Yetu: Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu? NO...

Elimu Yetu: Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu? NO...: Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu?    NO. 4 “Udongo uwahi ungali maji” ni msemo wa kawaida kabisa katika mazungumzo yet...

Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu? NO. 4



Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu?   NO. 4


“Udongo uwahi ungali maji” ni msemo wa kawaida kabisa katika mazungumzo yetu ya kila siku pale wazazi wanapohimizana katika kuanza mchakato wa kupeleka watoto zao shuleni. Tunafahamu kwamba kuna maisha ya elimu kwa watoto na pia kuna maisha ya elimu kwa vijana na watu wazima. Msemo wa “elimu haina mwisho” chanzo chake ni kuona hata watu wazima nao inafikia mahali wanaendelea na masomo kwa ngazi za juu zaidi. Si hivyo tu bali hata wanapojifunza mambo mapya ya kawaida katika maisha yao ya kila siku, naamini tunafahamu maana halisi ya neno elimu.
Ukipita katika shule mbalimbali utajionea maneno mbalimbali yanayotumika katika kuzungumzia umuhimu wa elimu. Wapo wanaokwambia “elimu ni ufunguo wa maisha” hapo unaweza kutafakari zaidi maana ya kauli hiyo? Kwamba ili uweze kuingia katika mlango wa ulimwengu wa kuishi vema kama wengine basi yafaa upate huo ufunguo wa gharama uitwao elimu. Naamini wengi wetu bado tunadhania kwamba elimu ni matayarisho kwa ajili ya maisha ya baadae, lakini ukweli wa jambo hilo hauko hivyo. Mwanazuoni wa kimarekani John Dewey alipata kusema ya kwamba “elimu ni maisha.”

Mwanadamu katika maisha yake anatawaliwa na nyanja mbalimbali za kimaisha ikiwemo na nyanja ya elimu, kwa hakika elimu ni jambo asilia kwa mwanadamu. Kila mwanadamu anazaliwa na kukua nalo jambo hilo, hivyo elimu ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Katika vitabu vitakatifu pia neno hilo limejitokeza mara kadhaa la kuwaasa wanadamu watafute maarifa kwa ajili ya maisha yao na vizazi vyao.


Kama unafuatilia vema maelezo yangu hoja yangu kuu hapo ni kwamba elimu ni maisha halisi na sio maandalizi kwa ajili ya maisha yajayo. Hivyo ni jukumu la wazazi na walezi kuhakikisha watoto zao wanaishi kwa kupitia na ulimwengu huo wa kielimu, kwa kuwapeleka watoto zao kujifunza masuala mbalimbali ya kuwasaidia katika maisha yao kwa wakati husika.
Elimu haipo kwa ajili ya kushindanisha watoto wala wazazi kujipatia fahari machoni mwa wazazi wengine, rejea katika makala ya kwanza kuhusu maana ya elimu na aina za elimu. Pia rejea makala ya pili na ya tatu kwa mwendelezo wa hoja ya elimu, maelezo ya kina katika makala hizo yanaweza kukupatia mwangaza ulio bora. Nimesema hapo awali kwamba elimu ni maisha hivyo si vibaya kama tunaweza pia kujiuliza maswali machache kuhusu maisha ya elimu kwa watoto, kama ifuatavyo;
·         Umri gani sahihi wa kumuanzisha mtoto shule?
·         Shule ipi sahihi kwa mtoto?
·         Elimu ipi itamfaa mtoto kwa umri wake?
·         Ni kwa kiasi gani tunafuatilia elimu ya watoto?
·         Ushirikiano gani tunatoa kwa walimu na walezi wa watoto?
·         Tunawapa nafasi kiasi gani watoto ya kucheza na wenzao?
Ni maswali yenye kuibua mjadala mzito na kwa hakika yana changamoto zake endapo utajaribu kuyajibu maswali hayo. Mabadiliko mengi yamekwisha tokea linapokuja suala la umri wa kumwanzisha mtoto shule, hapo awali ilipoanza elimu rasmi baada ya ujio wa wakoloni suala la umri halikuwa na mjadala kwani yeyote aliyekuwa anahitaji kusoma aliruhusiwa kusoma. Hali ikaendelea hivyo mpaka wakati tulipofanikiwa kupata uhuru wetu na kuwa na serikali yetu ndipo na mabadiliko mbalimbali yakaanza kutokea ili kukidhi matakwa ya mazingira kwa wakati huo.
Sera za elimu na hata sheria zikaanza kutungwa kwa ajili ya kuhakikisha mambo yanaenda vema katika jamii zetu, na katika kutunga sera hizo hata suala la umri likawa linaenda likibadilika toka miaka kumi ya kuanza darasa la kwanza kwa sasa imefikia umri wa miaka sita kuanza darasa la kwanza. Hivyo kabla ya kuanza darasa la kwanza mtoto anatakiwa kupitia katika madarasa ya awali, hapo ndipo pa kutazama zaidi kwani wazazi na walezi wengi wanachokifanya hapo sidhani kama wanazingatia utaalamu ama lah.
Tukumbuke shule ya kwanza kwa mtoto ni familia yake na jamii yake, hapo mtoto mbali ya kujifunza toka kwa wazazi na walezi pia anajifunza toka kwa watoto wenzie. Mtoto atajifunza kwa namna mbalimbali kwa kuona na hata kwa michezo yake na wenzie, hayo ni maisha ya mtoto huyo mdogo. Wazazi na walezi wengi wanajisahau pale wanapoanza kuishi maisha ya watoto wao ama kutamani watoto waishi maisha ya wao watu wazima. Kwa kudhania mtoto atawaza na kutenda kama atakavyo yeye mzazi ama mlezi.
Kila mtoto anapozaliwa anakuwa tayari na tabia alizozaliwa nazo kwa mujibu wa siku yake ya kuzaliwa, mtoto huyo tabia hizo ataweza kuzionesha vema akiwa na wenzie maana watoto huwa wana lugha yao na wana namna yao ya kuelewana. Watoto wanajifunza kwa kucheza zaidi kuliko namna nyingine yeyote ile.
Zaidi tuanze kubadili namna zetu za kufikiria kuhusu elimu za watoto wetu, ni sisi wa kuanza kutambu
a ukweli huu ya kwamba hatupeleki shule watoto ili waje kuajiriwa kama makarani ama matarishi. Huo ndio ulikuwa mfumo wa elimu ya kikoloni walipokuwa wanawaandaa waafrika ili wapate wasaidizi katika ofisi zao. Hivyo tusipeleke watoto shuleni kwa kuongozwa na wazo hilo kwamba baadae aje kuajiriwa kwa vile alisoma shule Fulani na anatambua lugha Fulani. Elimu ni kwa ajili ya watoto kupata taarifa na maarifa ya kizazi kilichopita, kilichopo na kubashiri kuhusu kizazi kijacho. Ili nao waweze kuwa chachu ya mabadiliko yao wenyewe na mabadiliko ya jamii yao.


Nb: Mada hii itakuwa na mwendelezo wake kwa kuendelea kujadili suala la elimu kwa mapana yake, ili wazazi na wadau wa elimu kupata nuru ya kufanya maamuzi sahihi.

Written by : Andrian Mkoba.

Saturday, January 24, 2015

Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu? NO. 3



Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu?   NO. 3
“Mtoto wa nyoka ni nyoka” Nitashangaa ukiniambia hujawahi kuusikia msemo huo katika pitapita zako ama wakati ukiwa mwanafunzi na wewe. Lakini nikikuuliza maana halisi ya msemo huo unaweza kunipa majibu mengi tofauti kwa kuwa hiyo imebeba lugha ya picha ndani yake. Nikisema lugha ya picha naomba nieleweke vema kwamba ni kauli ambayo imeficha ujumbe wake halisi, na kumuachia msomaji ama msikilizaji kuupatia maana yeye mwenyewe.

Lugha ni nini? Kuna maelezo mengi tofauti yanayoweza kuleta maana ya neno lugha, lakini itoshe kusema lugha ni chombo cha mawasiliano ambapo utokea kwa bahati nasibu ikiwa na lengo la kuwezesha mawasiliano kati ya mtu mmoja na mwingine ama kundi la watu. Watoto nao hawako nyuma katika matumizi ya lugha kama ilivyo katika makundi mengine ya watu.

Watoto huwa wanazaliwa wakiwa na uwezo maalum wa kutambua lugha ya mawasiliano katika jamii yao, kama mtaalam aliyebobea katika masuala ya lugha za dunia alivyopata kusema katika machapisho yake mbalimbali aliyofanya kuhusu lugha. Chomsky (1980)

Kila mtoto anazaliwa akiwa na uwezo wa kuelewa lugha, ni kama tulivyokwisha soma katika makala za awali namna elimu inavyoweza kupatikana. Unaweza kutafakari jambo hili ni mara ngapi umeshasikia watoto wadogo wajifunzao kuzungumza wakiita maji kwa jina la “MMA?” unaweza kuwa na majibu kwa swali hilo. Na endapo utakosa jibu basi nichukue nafasi hii kukusihi uwe unatumia muda wako kukaa jirani na watoto wajifunzao kuzungumza uweze kushuhudia namna wanavyofanana katika matamshi yao ya awali.

Lugha ni chombo cha mawasiliano wote tunaweza kukubaliana hivyo, watoto nao wanatumia lugha katika kuwasilisha mahitaji yao kwa wazazi na wale wanaowalea. Watoto wanajifunza lugha kwa njia mbalimbali katika mazingira yao. Ni changamoto kubwa sana kwa wazazi katika kuhakikisha watoto wanapata ufahamu wa lugha zinazotumika katika jamii yao.

Watoto wana nafasi kubwa kuliko kundi lingine lolote katika kujifunza lugha kwa vigezo mbalimbali, cha muhimu ni watoto kupewa nafasi na wazazi wao. Watoto wanatakiwa kupewa nafasi ya kucheza na wenzao kwa muda mrefu zaidi ili waweze kupata wakujifunza nao lugha yao. Maneno mapya wanaweza kuyapata wakiwa katika kundi la watoto wenzao ambapo maneno hayo wataenda kuwauliza wazazi wawapatie ufafanuzi.

Ili mtoto aweze kujifunza vema masuala yanayohusu jamii yake ni budi lugha ya jamii hiyo ifahamike kwa mtoto huyo, kuhusu namna gani mtoto anaweza kujifunza lugha ya jamii yake. Ufafanuzi nimeutoa hapo juu, hivyo ni wajibu wa wazazi na walezi kuwapa nafasi watoto ili kuweza kujifunza lugha kupitia kundi la watoto wenzao.

Jamii yetu na taifa linakumbwa na changamoto kubwa kwa sasa kuhusu uamuzi wa lugha ya kutumika katika kuelimisha watoto. Nawe unaweza kuwa kati ya wadau wa elimu ukiacha sifa yako ya uzazi ama ulezi, unaweza kushirikiana na jamii katika kushauriana lugha ifaayo katika kuelimishia watoto. Lengo likiwa ni kuwezesha watoto hao kupata maarifa na taarifa kusudiwa.

Lugha ambayo ndiyo inatumika katika mawasiliano ya jamii husika ndio ingekuwa chaguo la kwanza katika kutumika kuelimisha watoto. Si vibaya kujifunza na lugha nyingine za kigeni katika kumuwezesha mtoto kupata ufahamu wa lugha nyingine pia.

Lakini lengo la elimu ambalo ni kuhaulisha maarifa na taarifa toka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine ili litimie yumkini ikitumika lugha inayoeleweka kwa wote jambo hilo likafanikiwa. Tuonee fahari lugha ambayo watoto wetu wanaipenda na kuitumia kwa uhuru wakiwa na wenzao katika michezo yao inayowajenga kiakili na kimwili.

Tukumbuke lugha ni chombo cha mawasiliano, taarifa na maarifa yanaweza kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine kwa kutumia lugha. Lugha yenyewe si sehemu ya taarifa au maarifa hayo, nikiwa na maana mtu anaweza kuwa na uwezo wa kuifahamu lugha husika pasipo kuwa na maarifa wala taarifa sahihi kuhusu yaliyo muhimu kwa maendeleo yake.

Lugha isiwe kikwazo kwa kufanikisha suala la upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wetu ambao ndio wataalamu tunaotarajia waweze kuleta mabadiliko katika jamii zetu. Elimu ni nguvu kubwa kwa yeye aliyefanikiwa kuipata. Tuwape watoto nguvu hiyo kwa kuwapa taarifa na maarifa sahihi kwa kutumia lugha sahihi inayofanikisha upatikanaji wa elimu.

Tupo kwa ajili ya watoto, na ifahamike wazi bila ya watoto hakuna jamii wala taifa mahali popote. Tutimize wajibu wetu wa kufanikisha maendeleo ya watoto.

Nb: Mada hii itakuwa na mwendelezo wake kwa kuendelea kujadili suala la elimu kwa mapana yake, ili wazazi na wadau wa elimu kupata nuru ya kufanya maamuzi sahihi.

 WRITTEN BY: ANDRIAN MUKOBA.








Monday, January 19, 2015

Ubongo kids: Edutainment Africa



UBONGO KIDS: Huge efforts towards improving math and science in Tanzania.
     Have you heard of ubongo kids ?  There are tremendous efforts behind Tanzania miseries in education especially  Math and Science. Many of us failed the subjects but now I can feel my children will not. Apart from the horable stories from those who failed once impacted us negatively  and other reasons we did not find fun in Math and science .
        I think this project will change the future of education in Tanzania and Africa. Education  is core to any developing nation.  Its true that  children have lost the fun in learning and Ubongo kids is there to bring the fun back.

Kudos! Ubongo kids..

Monday, January 12, 2015

Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu? NO. 2



Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu?   NO. 2

“Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu” semi kama hiyo haina maana nyepesi kama inavyoweza kudhaniwa na mtu anapoisoma ama kuisikia ikitamkwa. Wanasaikolojia wa elimu na malezi wana elezea hatua mbalimbali za ukuaji wa binadamu kuanzia akiwa tumboni mwa mama, akizaliwa na akiendelea kukua.
Freud (1953) katika moja ya machapisho yake ametanabaisha funzo la kwanza kwa mtoto ni kupenda titi la mama yake. Nae mama wa mtoto anapofanya matendo mbalimbali kwa mwanae, ikiwemo kumnyonyesha, kumbusu, kumbembeleza, na kumsafisha anatekeleza jukumu lake la kimama la kumfundisha mtoto kuhusu upendo.

Usishangae ndugu msomaji kusikia suala la mama kumfundisha mwanae Upendo, nadhani kama tu-wasomaji wazuri wa maandiko matakatifu tunaweza kung’amua ya kwamba Mungu ni Upendo. Basi ili mtoto huyo aweze kweli kuwa kiumbe hai anastahili kupatiwa maarifa hayo ya namna ya kupenda kilicho sahihi kwake na kwa wengine.
 
Nguvu ya upendo ikiingia vema kwa mtoto itakuwa na mwendelezo mzuri sana wa kumkuza mtoto huyo, kwa kuwa kila jambo lifanyikalo katika maisha ya mwanadamu linaongozwa na upendo. Kama hakuna upendo tutarajie kinyume cha upendo ndio kishike hatamu ambacho si kingine bali ni chuki na uadui. Kumbe unaweza kuona hapo cha kwanza kilicho muhimu katika maisha ya mtoto ni Upendo.
Katika mada yangu ya awali, kumbuka nilitanabaisha namna mbalimbali za kupata elimu na nikasema kuna ngazi mbalimbali ambazo mtu anapitia katika kupata elimu akianzia ngazi ya familia. Msingi wa familia hiyo ni mama akisaidiana na baba, lakini pia jamii ya familia hiyo kwa ujumla wake ambao wanaweza kupata nafasi ya kuishi na mtoto.

Pia nilizungumza kwamba huwa inawezekana kwa mtu kujifunza baadhi ya mambo yeye mwenyewe, anajifunza mambo hayo kwa kuangalia namna wengine wanavyofanya. Kwa kupitia makundi rika, kusikiliza redio ama kutazama runinga. Hivyo si ajabu sana kuona mtoto akiwa na taarifa na maarifa Fulani ambayo wazazi na jamii inayomzunguka ni kitu kigeni kwao.

Ndipo ule msemo wetu “hasiyefunzwa na mamaye, ufunzwa na ulimwengu” unapoweza kuleta maana halisi kupitia maisha ya mtoto katika hatua zake za ukuaji atakazopitia. Wapo wanamuziki mbalimbali ndani na nje ya Tanzania ambao wamejaribu kutayarisha tungo madhubuti ya kumuhenzi mama. Wengine wakisema “Nani kama Mama?” kwa kupitia swali la tungo hizo za wanamuziki pia nawe unaweza kujiuliza baadhi ya maswali mengine yakiwemo haya yafuatayo;
·         Nani kama mama?
·         Kwanini nini iwe mama?
·         Baba ana nafasi gani?
·         Jamii ina nafasi gani?
·         Upendo ni nini na unafundishwaje?
·         Chuki ni nini na inafundishwaje?

Watoto kama ilivyo sisi tulipozaliwa, huwa wanazaliwa na hali ya udadisi. Huwa wanapenda kujua mambo mbalimbali kwanini yapo vile yalivyo ama kwanini yanaitwa vile. Ni kawaida sana kuona mtoto atokapo kucheza akimuuliza mama swali ama maswali tokana na jambo alilojifunza ama kulisikia toka kwa wenzie.
Ni jukumu la mama, baba na wale wote wanaoishi na mtoto huyo kumsikiliza maswali yake na kumpatia majibu muafaka pasipo kumdanganya. Endapo majibu ya maswali yake hatuna ni vema tukachukua jukumu la kutafuta majibu kwa wenzetu wanaofahamu ili tumpatie mtoto huyo jibu. Kwa namna hiyo ataendelea kujenga imani kubwa juu ya upendo wa wazazi na familia kwa ujumla. Na ataanza kujijengea hali ya kujiamini na kutamani na yeye kuwa mtu mwenye maarifa kama ilivyo kwa wazazi na wale wanaomzunguka.
Naamini umeona sasa ya kuwa si vema kumpatia mtoto jibu la uongo pale anapouliza, hakuna swali la kipuuzi analoweza kuuliza mtoto. Inawezekana kabisa ni wewe ukajipa tafsiri potofu kupitia swali madhubuti la mtoto. Mazungumzo yako na mtoto pale unapompatia majibu kwa maswali yake ndipo utakuwa unamwonesha upendo wako na namna ulivyo na maarifa. Haitashangaza kumsikia mtoto huyo akitamani yeye mwenyewe kwenda shule kwa kuwa anaanza kuona faida yake kupitia wewe mwenyewe kama mzazi.
Shule ya kwanza kwa mtoto ni familia yake, unapozungumza kuhusu familia yake ni mama na baba wa mtoto huyo. Ndipo wanafuatia ndugu na jamaa na marafiki wa mtoto huyo.

Kwa kujikumbusha tena, tumeumbwa na kuletwa hapa duniani lengo likiwa ni kuwa wana ELIMU. Kusaka maarifa kwa ajili ya kuifanya dunia mahali salama pa kuishi. Upendo ndio ulisababisha sisi tukaumbwa kwa namna tulivyo, upendo huo ndio unatufanya sisi tuendelee kuishi, kwa upendo huo huo tunastahili kuwafanyia wengine yaliyo ya upendo.

Nani kati yetu mwanae akimuomba kipande cha Samaki atampatia kipande cha Nyoka? Ni wazi hakuna mtu wa aina hiyo, lakini si ajabu akiwepo mtu wa aina hiyo pia. Endapo wakati wa ukuaji wake hakubahatika kupatiwa upendo wa mama na jamii iliyomzunguka. Katika hoja hii tutoke na wazo kuu la UPENDO tuufanyie kazi ili jamii ipate manufaa kwetu.

Nb: Mada hii itakuwa na mwendelezo wake kwa kuendelea kujadili suala la elimu kwa mapana yake, ili wazazi na wadau wa elimu kupata nuru ya kufanya maamuzi sahihi.