Monday, January 12, 2015

Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu? NO. 2



Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu?   NO. 2

“Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu” semi kama hiyo haina maana nyepesi kama inavyoweza kudhaniwa na mtu anapoisoma ama kuisikia ikitamkwa. Wanasaikolojia wa elimu na malezi wana elezea hatua mbalimbali za ukuaji wa binadamu kuanzia akiwa tumboni mwa mama, akizaliwa na akiendelea kukua.
Freud (1953) katika moja ya machapisho yake ametanabaisha funzo la kwanza kwa mtoto ni kupenda titi la mama yake. Nae mama wa mtoto anapofanya matendo mbalimbali kwa mwanae, ikiwemo kumnyonyesha, kumbusu, kumbembeleza, na kumsafisha anatekeleza jukumu lake la kimama la kumfundisha mtoto kuhusu upendo.

Usishangae ndugu msomaji kusikia suala la mama kumfundisha mwanae Upendo, nadhani kama tu-wasomaji wazuri wa maandiko matakatifu tunaweza kung’amua ya kwamba Mungu ni Upendo. Basi ili mtoto huyo aweze kweli kuwa kiumbe hai anastahili kupatiwa maarifa hayo ya namna ya kupenda kilicho sahihi kwake na kwa wengine.
 
Nguvu ya upendo ikiingia vema kwa mtoto itakuwa na mwendelezo mzuri sana wa kumkuza mtoto huyo, kwa kuwa kila jambo lifanyikalo katika maisha ya mwanadamu linaongozwa na upendo. Kama hakuna upendo tutarajie kinyume cha upendo ndio kishike hatamu ambacho si kingine bali ni chuki na uadui. Kumbe unaweza kuona hapo cha kwanza kilicho muhimu katika maisha ya mtoto ni Upendo.
Katika mada yangu ya awali, kumbuka nilitanabaisha namna mbalimbali za kupata elimu na nikasema kuna ngazi mbalimbali ambazo mtu anapitia katika kupata elimu akianzia ngazi ya familia. Msingi wa familia hiyo ni mama akisaidiana na baba, lakini pia jamii ya familia hiyo kwa ujumla wake ambao wanaweza kupata nafasi ya kuishi na mtoto.

Pia nilizungumza kwamba huwa inawezekana kwa mtu kujifunza baadhi ya mambo yeye mwenyewe, anajifunza mambo hayo kwa kuangalia namna wengine wanavyofanya. Kwa kupitia makundi rika, kusikiliza redio ama kutazama runinga. Hivyo si ajabu sana kuona mtoto akiwa na taarifa na maarifa Fulani ambayo wazazi na jamii inayomzunguka ni kitu kigeni kwao.

Ndipo ule msemo wetu “hasiyefunzwa na mamaye, ufunzwa na ulimwengu” unapoweza kuleta maana halisi kupitia maisha ya mtoto katika hatua zake za ukuaji atakazopitia. Wapo wanamuziki mbalimbali ndani na nje ya Tanzania ambao wamejaribu kutayarisha tungo madhubuti ya kumuhenzi mama. Wengine wakisema “Nani kama Mama?” kwa kupitia swali la tungo hizo za wanamuziki pia nawe unaweza kujiuliza baadhi ya maswali mengine yakiwemo haya yafuatayo;
·         Nani kama mama?
·         Kwanini nini iwe mama?
·         Baba ana nafasi gani?
·         Jamii ina nafasi gani?
·         Upendo ni nini na unafundishwaje?
·         Chuki ni nini na inafundishwaje?

Watoto kama ilivyo sisi tulipozaliwa, huwa wanazaliwa na hali ya udadisi. Huwa wanapenda kujua mambo mbalimbali kwanini yapo vile yalivyo ama kwanini yanaitwa vile. Ni kawaida sana kuona mtoto atokapo kucheza akimuuliza mama swali ama maswali tokana na jambo alilojifunza ama kulisikia toka kwa wenzie.
Ni jukumu la mama, baba na wale wote wanaoishi na mtoto huyo kumsikiliza maswali yake na kumpatia majibu muafaka pasipo kumdanganya. Endapo majibu ya maswali yake hatuna ni vema tukachukua jukumu la kutafuta majibu kwa wenzetu wanaofahamu ili tumpatie mtoto huyo jibu. Kwa namna hiyo ataendelea kujenga imani kubwa juu ya upendo wa wazazi na familia kwa ujumla. Na ataanza kujijengea hali ya kujiamini na kutamani na yeye kuwa mtu mwenye maarifa kama ilivyo kwa wazazi na wale wanaomzunguka.
Naamini umeona sasa ya kuwa si vema kumpatia mtoto jibu la uongo pale anapouliza, hakuna swali la kipuuzi analoweza kuuliza mtoto. Inawezekana kabisa ni wewe ukajipa tafsiri potofu kupitia swali madhubuti la mtoto. Mazungumzo yako na mtoto pale unapompatia majibu kwa maswali yake ndipo utakuwa unamwonesha upendo wako na namna ulivyo na maarifa. Haitashangaza kumsikia mtoto huyo akitamani yeye mwenyewe kwenda shule kwa kuwa anaanza kuona faida yake kupitia wewe mwenyewe kama mzazi.
Shule ya kwanza kwa mtoto ni familia yake, unapozungumza kuhusu familia yake ni mama na baba wa mtoto huyo. Ndipo wanafuatia ndugu na jamaa na marafiki wa mtoto huyo.

Kwa kujikumbusha tena, tumeumbwa na kuletwa hapa duniani lengo likiwa ni kuwa wana ELIMU. Kusaka maarifa kwa ajili ya kuifanya dunia mahali salama pa kuishi. Upendo ndio ulisababisha sisi tukaumbwa kwa namna tulivyo, upendo huo ndio unatufanya sisi tuendelee kuishi, kwa upendo huo huo tunastahili kuwafanyia wengine yaliyo ya upendo.

Nani kati yetu mwanae akimuomba kipande cha Samaki atampatia kipande cha Nyoka? Ni wazi hakuna mtu wa aina hiyo, lakini si ajabu akiwepo mtu wa aina hiyo pia. Endapo wakati wa ukuaji wake hakubahatika kupatiwa upendo wa mama na jamii iliyomzunguka. Katika hoja hii tutoke na wazo kuu la UPENDO tuufanyie kazi ili jamii ipate manufaa kwetu.

Nb: Mada hii itakuwa na mwendelezo wake kwa kuendelea kujadili suala la elimu kwa mapana yake, ili wazazi na wadau wa elimu kupata nuru ya kufanya maamuzi sahihi.

1 comment: