Saturday, January 31, 2015

Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu? NO. 4



Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu?   NO. 4


“Udongo uwahi ungali maji” ni msemo wa kawaida kabisa katika mazungumzo yetu ya kila siku pale wazazi wanapohimizana katika kuanza mchakato wa kupeleka watoto zao shuleni. Tunafahamu kwamba kuna maisha ya elimu kwa watoto na pia kuna maisha ya elimu kwa vijana na watu wazima. Msemo wa “elimu haina mwisho” chanzo chake ni kuona hata watu wazima nao inafikia mahali wanaendelea na masomo kwa ngazi za juu zaidi. Si hivyo tu bali hata wanapojifunza mambo mapya ya kawaida katika maisha yao ya kila siku, naamini tunafahamu maana halisi ya neno elimu.
Ukipita katika shule mbalimbali utajionea maneno mbalimbali yanayotumika katika kuzungumzia umuhimu wa elimu. Wapo wanaokwambia “elimu ni ufunguo wa maisha” hapo unaweza kutafakari zaidi maana ya kauli hiyo? Kwamba ili uweze kuingia katika mlango wa ulimwengu wa kuishi vema kama wengine basi yafaa upate huo ufunguo wa gharama uitwao elimu. Naamini wengi wetu bado tunadhania kwamba elimu ni matayarisho kwa ajili ya maisha ya baadae, lakini ukweli wa jambo hilo hauko hivyo. Mwanazuoni wa kimarekani John Dewey alipata kusema ya kwamba “elimu ni maisha.”

Mwanadamu katika maisha yake anatawaliwa na nyanja mbalimbali za kimaisha ikiwemo na nyanja ya elimu, kwa hakika elimu ni jambo asilia kwa mwanadamu. Kila mwanadamu anazaliwa na kukua nalo jambo hilo, hivyo elimu ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Katika vitabu vitakatifu pia neno hilo limejitokeza mara kadhaa la kuwaasa wanadamu watafute maarifa kwa ajili ya maisha yao na vizazi vyao.


Kama unafuatilia vema maelezo yangu hoja yangu kuu hapo ni kwamba elimu ni maisha halisi na sio maandalizi kwa ajili ya maisha yajayo. Hivyo ni jukumu la wazazi na walezi kuhakikisha watoto zao wanaishi kwa kupitia na ulimwengu huo wa kielimu, kwa kuwapeleka watoto zao kujifunza masuala mbalimbali ya kuwasaidia katika maisha yao kwa wakati husika.
Elimu haipo kwa ajili ya kushindanisha watoto wala wazazi kujipatia fahari machoni mwa wazazi wengine, rejea katika makala ya kwanza kuhusu maana ya elimu na aina za elimu. Pia rejea makala ya pili na ya tatu kwa mwendelezo wa hoja ya elimu, maelezo ya kina katika makala hizo yanaweza kukupatia mwangaza ulio bora. Nimesema hapo awali kwamba elimu ni maisha hivyo si vibaya kama tunaweza pia kujiuliza maswali machache kuhusu maisha ya elimu kwa watoto, kama ifuatavyo;
·         Umri gani sahihi wa kumuanzisha mtoto shule?
·         Shule ipi sahihi kwa mtoto?
·         Elimu ipi itamfaa mtoto kwa umri wake?
·         Ni kwa kiasi gani tunafuatilia elimu ya watoto?
·         Ushirikiano gani tunatoa kwa walimu na walezi wa watoto?
·         Tunawapa nafasi kiasi gani watoto ya kucheza na wenzao?
Ni maswali yenye kuibua mjadala mzito na kwa hakika yana changamoto zake endapo utajaribu kuyajibu maswali hayo. Mabadiliko mengi yamekwisha tokea linapokuja suala la umri wa kumwanzisha mtoto shule, hapo awali ilipoanza elimu rasmi baada ya ujio wa wakoloni suala la umri halikuwa na mjadala kwani yeyote aliyekuwa anahitaji kusoma aliruhusiwa kusoma. Hali ikaendelea hivyo mpaka wakati tulipofanikiwa kupata uhuru wetu na kuwa na serikali yetu ndipo na mabadiliko mbalimbali yakaanza kutokea ili kukidhi matakwa ya mazingira kwa wakati huo.
Sera za elimu na hata sheria zikaanza kutungwa kwa ajili ya kuhakikisha mambo yanaenda vema katika jamii zetu, na katika kutunga sera hizo hata suala la umri likawa linaenda likibadilika toka miaka kumi ya kuanza darasa la kwanza kwa sasa imefikia umri wa miaka sita kuanza darasa la kwanza. Hivyo kabla ya kuanza darasa la kwanza mtoto anatakiwa kupitia katika madarasa ya awali, hapo ndipo pa kutazama zaidi kwani wazazi na walezi wengi wanachokifanya hapo sidhani kama wanazingatia utaalamu ama lah.
Tukumbuke shule ya kwanza kwa mtoto ni familia yake na jamii yake, hapo mtoto mbali ya kujifunza toka kwa wazazi na walezi pia anajifunza toka kwa watoto wenzie. Mtoto atajifunza kwa namna mbalimbali kwa kuona na hata kwa michezo yake na wenzie, hayo ni maisha ya mtoto huyo mdogo. Wazazi na walezi wengi wanajisahau pale wanapoanza kuishi maisha ya watoto wao ama kutamani watoto waishi maisha ya wao watu wazima. Kwa kudhania mtoto atawaza na kutenda kama atakavyo yeye mzazi ama mlezi.
Kila mtoto anapozaliwa anakuwa tayari na tabia alizozaliwa nazo kwa mujibu wa siku yake ya kuzaliwa, mtoto huyo tabia hizo ataweza kuzionesha vema akiwa na wenzie maana watoto huwa wana lugha yao na wana namna yao ya kuelewana. Watoto wanajifunza kwa kucheza zaidi kuliko namna nyingine yeyote ile.
Zaidi tuanze kubadili namna zetu za kufikiria kuhusu elimu za watoto wetu, ni sisi wa kuanza kutambu
a ukweli huu ya kwamba hatupeleki shule watoto ili waje kuajiriwa kama makarani ama matarishi. Huo ndio ulikuwa mfumo wa elimu ya kikoloni walipokuwa wanawaandaa waafrika ili wapate wasaidizi katika ofisi zao. Hivyo tusipeleke watoto shuleni kwa kuongozwa na wazo hilo kwamba baadae aje kuajiriwa kwa vile alisoma shule Fulani na anatambua lugha Fulani. Elimu ni kwa ajili ya watoto kupata taarifa na maarifa ya kizazi kilichopita, kilichopo na kubashiri kuhusu kizazi kijacho. Ili nao waweze kuwa chachu ya mabadiliko yao wenyewe na mabadiliko ya jamii yao.


Nb: Mada hii itakuwa na mwendelezo wake kwa kuendelea kujadili suala la elimu kwa mapana yake, ili wazazi na wadau wa elimu kupata nuru ya kufanya maamuzi sahihi.

Written by : Andrian Mkoba.

0 comments:

Post a Comment