Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani zetu? NO. 3
“Mtoto wa nyoka ni nyoka”
Nitashangaa ukiniambia hujawahi kuusikia msemo huo katika pitapita zako ama
wakati ukiwa mwanafunzi na wewe. Lakini nikikuuliza maana halisi ya msemo huo
unaweza kunipa majibu mengi tofauti kwa kuwa hiyo imebeba lugha ya picha ndani
yake. Nikisema lugha ya picha naomba nieleweke vema kwamba ni kauli ambayo
imeficha ujumbe wake halisi, na kumuachia msomaji ama msikilizaji kuupatia
maana yeye mwenyewe.
Lugha ni nini? Kuna maelezo mengi
tofauti yanayoweza kuleta maana ya neno lugha, lakini itoshe kusema lugha ni
chombo cha mawasiliano ambapo utokea kwa bahati nasibu ikiwa na lengo la
kuwezesha mawasiliano kati ya mtu mmoja na mwingine ama kundi la watu. Watoto
nao hawako nyuma katika matumizi ya lugha kama ilivyo katika makundi mengine ya
watu.
Watoto huwa wanazaliwa wakiwa na
uwezo maalum wa kutambua lugha ya mawasiliano katika jamii yao, kama mtaalam
aliyebobea katika masuala ya lugha za dunia alivyopata kusema katika machapisho
yake mbalimbali aliyofanya kuhusu lugha. Chomsky (1980)
Kila mtoto anazaliwa akiwa na
uwezo wa kuelewa lugha, ni kama tulivyokwisha soma katika makala za awali namna
elimu inavyoweza kupatikana. Unaweza kutafakari jambo hili ni mara ngapi
umeshasikia watoto wadogo wajifunzao kuzungumza wakiita maji kwa jina la “MMA?”
unaweza kuwa na majibu kwa swali hilo. Na endapo utakosa jibu basi nichukue
nafasi hii kukusihi uwe unatumia muda wako kukaa jirani na watoto wajifunzao
kuzungumza uweze kushuhudia namna wanavyofanana katika matamshi yao ya awali.
Lugha ni chombo cha mawasiliano
wote tunaweza kukubaliana hivyo, watoto nao wanatumia lugha katika kuwasilisha
mahitaji yao kwa wazazi na wale wanaowalea. Watoto wanajifunza lugha kwa njia
mbalimbali katika mazingira yao. Ni changamoto kubwa sana kwa wazazi katika
kuhakikisha watoto wanapata ufahamu wa lugha zinazotumika katika jamii yao.
Watoto wana nafasi kubwa kuliko
kundi lingine lolote katika kujifunza lugha kwa vigezo mbalimbali, cha muhimu
ni watoto kupewa nafasi na wazazi wao. Watoto wanatakiwa kupewa nafasi ya
kucheza na wenzao kwa muda mrefu zaidi ili waweze kupata wakujifunza nao lugha
yao. Maneno mapya wanaweza kuyapata wakiwa katika kundi la watoto wenzao ambapo
maneno hayo wataenda kuwauliza wazazi wawapatie ufafanuzi.
Ili mtoto aweze kujifunza vema
masuala yanayohusu jamii yake ni budi lugha ya jamii hiyo ifahamike kwa mtoto
huyo, kuhusu namna gani mtoto anaweza kujifunza lugha ya jamii yake. Ufafanuzi
nimeutoa hapo juu, hivyo ni wajibu wa wazazi na walezi kuwapa nafasi watoto ili
kuweza kujifunza lugha kupitia kundi la watoto wenzao.
Jamii yetu na taifa linakumbwa na
changamoto kubwa kwa sasa kuhusu uamuzi wa lugha ya kutumika katika kuelimisha
watoto. Nawe unaweza kuwa kati ya wadau wa elimu ukiacha sifa yako ya uzazi ama
ulezi, unaweza kushirikiana na jamii katika kushauriana lugha ifaayo katika
kuelimishia watoto. Lengo likiwa ni kuwezesha watoto hao kupata maarifa na
taarifa kusudiwa.
Lugha ambayo ndiyo inatumika
katika mawasiliano ya jamii husika ndio ingekuwa chaguo la kwanza katika
kutumika kuelimisha watoto. Si vibaya kujifunza na lugha nyingine za kigeni
katika kumuwezesha mtoto kupata ufahamu wa lugha nyingine pia.
Lakini lengo la elimu ambalo ni
kuhaulisha maarifa na taarifa toka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine ili
litimie yumkini ikitumika lugha inayoeleweka kwa wote jambo hilo likafanikiwa. Tuonee
fahari lugha ambayo watoto wetu wanaipenda na kuitumia kwa uhuru wakiwa na
wenzao katika michezo yao inayowajenga kiakili na kimwili.
Tukumbuke lugha ni chombo cha
mawasiliano, taarifa na maarifa yanaweza kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu
mwingine kwa kutumia lugha. Lugha yenyewe si sehemu ya taarifa au maarifa hayo,
nikiwa na maana mtu anaweza kuwa na uwezo wa kuifahamu lugha husika pasipo kuwa
na maarifa wala taarifa sahihi kuhusu yaliyo muhimu kwa maendeleo yake.
Lugha isiwe kikwazo kwa
kufanikisha suala la upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wetu ambao ndio
wataalamu tunaotarajia waweze kuleta mabadiliko katika jamii zetu. Elimu ni
nguvu kubwa kwa yeye aliyefanikiwa kuipata. Tuwape watoto nguvu hiyo kwa kuwapa
taarifa na maarifa sahihi kwa kutumia lugha sahihi inayofanikisha upatikanaji
wa elimu.
Tupo kwa ajili ya watoto, na
ifahamike wazi bila ya watoto hakuna jamii wala taifa mahali popote. Tutimize
wajibu wetu wa kufanikisha maendeleo ya watoto.
Nb: Mada hii itakuwa na
mwendelezo wake kwa kuendelea kujadili suala la elimu kwa mapana yake, ili
wazazi na wadau wa elimu kupata nuru ya kufanya maamuzi sahihi.
WRITTEN BY: ANDRIAN MUKOBA.
0 comments:
Post a Comment