Sunday, March 15, 2015

ELIMU; SILAHA ITAKAYOTUWEZESHA KUPAMBANA NA MAADUI WATATU.



Na Makirita Amani.



Rais wa kwanza a Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema kwamba ili tuendelee tunahitaji kupambana na maadui watatu wa maendeleo. Na alitaja maadui hao ni UJINGA, MARADHI na UMASIKINI.

Pamoja na miaka mingi kupita tokea kutolewa kwa kauli hiyo bado ktolewa, bado maadui hawa watatu wanatusumbua sana kama taifa. Tunaona jinsi ambavyo ujinga unaendelea kuturudisha nyuma kama taifa. Pamoja na kujengwa kwa shule nyingi bado sehemu kubwa ya watanzania hawana elimu ya kutosha kuwaondolea ujunga. Tunaona jinsi ambavyo maradhi yanayoweza kuzuilika yanavyopoteza maisha ya wananchi wengi. Na pia tunaona jinsi ambavyo umasikini unaendelea kukithiri na maisha kuwa magumu kwa wananchi wengi.
Kuna silaha moja ambayo kama ikitumiwa vizuri inaweza kupambana na maadui hawa watatu. Silaha hiyo ina nguvu kubwa sana ambayo inaweza kuleta mabadiliko makubwa sana kwenye taifa letu na hatimaye tukaweza kufikia maendeleo makubwa. Silaha hiyo ni ELIMU.
Elimu ni silaha muhimu na kama ikiweza kutumiwa vizuri inaweza kutokomeza kabisa maadui hawa watatu.

Ni kwa jinsi gani elimu inaweza kupambana na maadui hawa watatu?

UJINGA.
Ujinga unatokana moja kwa moja na ukosefu wa elimu. Pale watu wanapokose elimu kuhusu jambo fulani hubaki kuwa wajinga kuhusiana na jambo hilo. Pale watu wanaposhindwa kujua matumizi mazuri ya rasilimali zao huo ni ujunga.
Kama watu wakipewa elimu itakayowasaidia kujitambua na kuelewa mambo yanayowahusu itawaondolea ujinga na kuwawezesha kushiriki kikamilifu kwenye maendelo yao wenyewe na maendeleo ya taifa.
Elimu ni muhimu sana kwenye kupambana na ujinga.

MARADHI.
Sehemu kubwa ya maradhi yanayotusumbua na kupoteza maisha ya watu wengi ni maradhi ya kuambukiza. Maradhi kama malaria, kipindupindu, ukimwi, kifua kikuu na hata kichocho ni maradhi ambayo yanaambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Kama watu wakipata elimu sahihi wanaweza kujikinga wasiambukizwe magonjwa haya. Na hata wale ambao wanapata magonjwa haya kwa kupata elimu sahihi wanaweza kujizuia wasiambukize wengine.
Elimu sahihi itatuwezesha kujikinga na maradhi na pia itawezesha wataalamu wa afya kugundua dawa na chanjo za maradhi haya hatarishi.

UMASIKINI.
Tatizo kubwa la umasikini tulilonalo kwenye nchi yetu linatokana na ukosefu wa elimu. Tuna rasilimali nyingi sana lakini hatuwezi kuzitumia kwa sababu ya ukosefu wa elimu. Leo hii tuna madini, mafuta na hata gesi lakini inabidi tutafute wawekezaji kutoka nchi zilizoendelea ndio wachimbe rasilimali hizi. Kwa njia hii rasilimali zetu zinanufaisha mataifa mengine kuliko zinavyotunufaisha sisi. Kama wananchi wangekuwa wamepata elimu sahihi ya kuwawezesha kutumia rasilimali hizi tungekuwa tumepaga hatua kubwa sana kimaendeleo.
Ili kuondokana na umasikini elimu ni muhimu sana. Na hata maradhi ambayo yanatusumbua sana nayo yanachangia kwenye umasikini wetu. Fedha nyingi zinapelekwa kwenye kuhudumia wagonjwa ambao wangeweza kujizuia wasipate magonjwa hayo kama wangekuwa na elimu sahihi.

Elimu ni muhimu sana kwenye maendeleo ya taifa lolote. Ili kupambana na maadui watatu wa maendeleo, elimu ndio silaha namba moja na inayoweza kuwaangamiza. Tuboreshe elimu yetu na tuhakikishe inawafikia watu wengi zaidi ili kuweza kuleta mabadiliko katika nchi yetu. Tunahitaji kukazana zaidi na kuongeza kasi kwenye maendeleo ya elimu ili kupunguza muda tunaopoteza kwenye umasikini.

1 comment:

  1. nadhani kwa sasa kuna adui mwingine rushwa au wale watu weupe wanasema kuwa ni corruption .. hii inaonesha kuwa ni kwamba kwakweli tunaitaji kuboresha mbinu zetu kam kweli utakubaliana na mie kuwa hata huyo ni adui wetu asa iv .. hvyo ahatuwezi tumia mbinu zile zile kwenye matatizo yaleyle .. mana watu wazamani walisema kuwa kutumia mbinu zilezile kutatua matatizo yaleyale ni sawa na kusukuma maji na km ukimwuliza mrisho mpoto nadhani atakwambia kuwa huo ni ujinga ... na hapo utakubaliana na mie kuwa tutakuwa tunatumia tatizo kukabiliana na matatizo mengi zaid ... Nyerere was da best na inawezekana actokee km yy tena .. ila kwakweli nadhani inabdi tuanzie pale alipotuachia tuboreshe kidogo na tuendelee mbele mana maisha haya lazima kuwe na mabadiliko kwakweli ... !!1 maoni yangu tu

    ReplyDelete