“Mazingira magumu” neno mazingira
pia lina maelezo mengine yakufanana nalo ambayo ni mandhari, hali, zunguka,
zingira, zingia, na zinga. Hivyo “magumu” ni kivumishi cha kuoneshea ni kwa
namna gani hayo mazingira yalivyo. Kama ukisema ni hali ngumu pia inaendana na
dhana nzima ya mazingira magumu katika hoja yangu ya msingi.
Mazingira magumu huwa
yanatofautiana kati ya kaya moja na kaya nyingine, watoto wanaoishi katika
mazingira magumu wana tofautiana pia katika hali wanazopitia katika maisha yao.
Kupata wazazi au walezi wasiothamini elimu wala kuona umuhimu wa watoto kupata
elimu, ni mazingira magumu ya awali ambayo kwa namna ya kipekee hayawezi kumpa
mtoto hamasa ya kupenda kusoma.
Katika makala zilizotangulia
niligusia suala zima la upendo wa wazazi kwa mtoto, mama na baba na ndugu wa
karibu wa familia wana nafasi kubwa katika kumjengea mtoto mazingira mepesi
kuelekea mafanikio yake ya kielimu. Tukumbuke watoto wanazaliwa wakiwa na uwezo
wa kiakili na ufahamu wa kiasi tayari kwa kuanza kujifunza mambo mengine kadiri
ya mazingira atakayokutana nayo.
Agizo kuu la awali la Mungu kwa
Adamu na Eva ilikuwa ni la kuzaa na kuongezeka ili wapate kuijaza dunia, hivyo
uwepo wetu hapa duniani wa mtu mke na mtu mume ni katika kutimiliza upendo huo
mkuu toka kwa Mungu. “Kuzaa si kazi, kazi kulea mwana” ni msemo wa kawaida sana
kuusikia linapokuja suala la mjadala kuhusu watoto na malezi yao. Tatizo kubwa
lililopo ni kwenye tafsiri ya maneno yanayotumika katika suala zima la
mawasiliano, ukichukulia kauli hiyo ya kazi kulea mwana kila mmoja anaweza kuwa
na fikra tofauti lakini mimi naweza kukwambia kulea ililenga katika dhana ya
kumwelimisha mtoto.
Mungu ndiye chanzo cha maarifa
yote, Mungu ni hekima ipitayo hekima zote katika kuona ukweli huo katika kitabu
kitakatifu cha Biblia katika kitabu cha Mithali, “Watu wangu wanaangamia kwa
kukosa maarifa” ni kauli aliyotoa Mwenyezi Mungu ikionesha umuhimu wa maarifa
ili watu wa Mungu wasiangamie. Katika hili ndipo wazo la Baba na Mama ni miungu
wa dunia usije kulisahau na kulipuuzia. Kwani Baba na Mama ni wa kwanza katika
kuhakikisha mtoto wao anapata maarifa stahiki, nadhani ndugu msomaji umeanza
kupata picha sasa ya namna ya kutenda kadiri inavyopasa.
Mazingira magumu yanaweza
kufanana na haya yafuatayo, mtoto kutozungukwa na watu wenye mwamko wa kielimu,
ikiwemo mtoto kuzaliwa katika ukoo usio na mwamko wa kielimu, mtoto kuzaliwa
katika familia hohehahe yenye kipato duni kisichotosheleza hata kupata mlo wa
siku moja. Mtoto kulelewa na mzazi mmoja iwe baba au mama, mtoto kulelewa na
bibi na babu, mtoto kulelewa na ndugu na jamaa, mtoto kuzaliwa katika eneo
lenye utamaduni usiojali elimu, mtoto kuzaliwa katika eneo lenye mtazamo hasi
kuhusu masuala ya kielimu, mtoto kuzaliwa katika wakati ambao Taifa halina
mwelekeo mzuri wa kielimu wala mipango ya kujikwamua katika kuwekeza kwenye
elimu ya watoto. Hiyo ni mifano ya baadhi tu ya mazingira magumu ambayo
yanachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya kielimu ya mtoto.
Kila aina ya mfano wa
mazingira magumu unaweza kupata maelezo mengi tofauti kwa kuwa namna ya
kukabiliana na mazingira hayo pia inatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Jambo
la msingi kabisa ni mwamko wa kielimu wa jamii husika ambayo mtoto huyo atakuwa
amezaliwa. Jamii hiyo inachukuliaje suala zima la elimu? Kwa namna ya kipekee
katika hoja hii nitapenda kuelezea pia na uzoefu wangu katika maisha haya
tunayoweza kuita ya mazingira magumu.
Kijana “Kung’alo” jina la
kubuni, ni mzaliwa wa kaya duni kama zilivyo kaya nyingi za hapa Tanzania amepitia
katika mazingira mengi magumu ya kimaisha. Lakini kwa upendo na msaada mkubwa
wa Mungu ameweza kujifunza masuala mbalimbali ya kijamii. Katika familia yao walizaliwa watoto takriban
nane (8) katika jiji la Dar es salaam, jiji lililojaa kila aina ya pilika tangu
enzi za utawala wa awamu ya kwanza baada ya kupata uhuru.
Wazazi wao hawakuwa waajiriwa,
ni baba ndio alikuwa chanzo cha kipato cha familia kwa hivyo kulikuwa na
changamoto mbalimbali katika maisha ya familia hiyo. Kung’alo akingali mdogo
yeye na ndugu zake baba yao alianza kuingia katika ulevi wa kupindukia ambao
kwa namna kubwa ulisababisha kuyumba kwa familia kwani kipato kidogo alichokuwa
akipata baba huyo, pia kilifanyiwa matumizi mengine ya anasa za dunia.
Wakati wa kuanza kujiunga na
shule ulipowadia kadiri ya umri wa Kung’alo ambaye ndie alikuwa wa kwanza
kuzaliwa alienda kuanza darasa la kwanza. Wakati huo umri wa kuanza darasa la
kwanza ilikuwa ni miaka 9 na 10, akawa na maendeleo mazuri darasani alipofika
darasa la tatu na mdogo wake Kung’alo alianzishwa darasa la kwanza na yeye.
Familia hiyo ilikuwa na utaratibu huo wa kuwapishanisha madarasa mawili watoto
wao ikishabihiana na tofauti yao ya umri wa kuzaliwa.
Watoto wa kaya hiyo walikuwa
na uwezo mkubwa wa kiakili kwani walikuwa na maendeleo mazuri katika masomo yao
tangu ngazi ya awali. Maisha yao yakazidi kuwa magumu kwa vile sasa mahitaji
yakawa mengi zaidi yakiongezeka na gharama za shule, kwani ili watoto waendelee
vema na masomo kuna wakati walilazimika kwenda twisheni na kufanya mitihani
mbalimbali ya majaribio. Kwa hakika pongezi kubwa inastahili kwenda kwa mama
yao mzazi bwana Kung’alo na wadogo zake. Mama huyo alihakikisha watoto zake
wanapata elimu, alikuwa na juhudi kubwa ya kufuatilia mwenendo wa watoto zake.
Mama huyo alikuwa na utaratibu
wa kuwatambua walimu wa darasa kwa kila mtoto wake, hivyo kwa utaratibu huo
aliweza kufahamiana na walimu wengi sana shuleni walipokuwa wanasoma watoto
zake. Jambo la kipekee ni kwamba mama huyo aliamua watoto zake wote wasome
katika shule hiyo hiyo, nadhani akiwa na lengo madhubuti la kuwafuatilia kwa
ukaribu zaidi kuliko wangekuwa kila mmoja anasoma katika shule tofauti.
Alishiriki kila kikao cha wazazi wa wanafunzi pale walipokuwa wanahitajika
kufika shuleni kusikiliza mipango ya shule hiyo.
Wakati wote huo baba yao kina
Kung’alo yeye alikuwa akiendelea na mabadiliko yake ya maisha ya anasa ilhali
kipato chake pia hakikuwa cha kuridhisha. Kadiri hali ilivyozidi kuwa ngumu,
ndipo mama yao kina Kung’alo akaanza kujishughulisha na biashara mbalimbali
ndogondogo katika jitihada za kupunguza ugumu wa maisha na kupata pesa za
kusaidia maendeleo ya watoto shuleni. Kung’alo na wadogo zake nao hawakuwa
nyuma wakisaidiana na mama yao katika kutafuta ridhki kwa ajili ya mahitaji ya
familia. Mungu akaendelea kuwajalia vijana hao, wakaendelea vema na masomo yao
bila ya kukatishwa tamaa na mazingira waliyokuwa nayo.
Kung’alo alifanikiwa kufaulu
vema katika mitihani yake ya darasa la saba na kuchaguliwa kwenda sekondari,
kwa wakati huo jambo kama hilo lilikuwa ni la kipekee waliokuwa wanafaulu na
kuchaguliwa walistahili kwelikweli kwa vile walikuwa na akili na vipaji sana.
Na kwa hali ya ufinyu wa shule kwa wakati ule idadi ya waliochaguliwa ilikuwa
ni ndogo sana, lakini haikuwa kwa kijana huyo Kung’alo.
Ikawa hivyo hivyo na kwa
wadogo zake Kung’alo walifanikiwa kupata nafasi ya kuendelea na elimu ya
sekondari, ikawa ni furaha kubwa kwa mama yao hasa juhudi kubwa aliyoifanya
kuhakikisha watoto zake wanasoma. Baba yao alikuwa akijivunia vipaji vya watoto
hao kwa kujinadi kuwa amefanikiwa kuwasomesha watoto zake, kinyume na hali
ilivyokuwa kwani ni mama yao ndio alikuwa shujaa wa elimu yao. Hata walipokuwa
wakilala bila ya kula mlo wa usiku lakini bado vijana hao walilazimika kuamka
mapema na kuwahi namba shuleni.
Ni kama walitambua kwamba
elimu ndio itakuwa mkombozi wa familia yao kwa siku zijazo, walikuwa na juhudi
kubwa ya kusoma wakichagizwa na uwezo mkubwa wa kiakili waliozaliwa nao.
Mazingira mbalimbali ya kukatisha tamaa walikumbana nayo ikiwemo ya kukosa
chakula iwe asubuhi, mchana na usiku lakini linapokuja suala la shule walikuwa
mstari wa mbele. Walikosa pesa ya kulipia twisheni, walikosa ada, upatikanaji
wa ada ulikuwa ni wa kukatisha tamaa walipokuwa katika shule za sekondari
lakini waliendelea kupenda elimu.
Kuzaliwa katika mazingira
magumu sio kigezo pekee cha mtoto kushindwa kufanya vema katika masomo yake,
lazima viwepo vichocheo vingine vya kufanya ugumu huo ukawa kikwazo. Katika
maelezo yote ya makali hii ukiangalia unagundua kwamba huwezi kufanya jambo
lolote pasipo kuwa na sehemu ya kusimamia. Hata wajenzi wa nyumba huwa wanaanza
na msingi katika kusimamisha jengo lao, ndivyo ilivyo kwa mtoto anayezaliwa
katika mazingira magumu ili aweze kuendelea vema ni budi apate sehemu ya
kusimamia.
Kuwepo na mtu wa kumsimamia na
kumwongoza, ni kweli wapo wanaozaliwa na kipaji cha kujipa motisha na hamasa wao
wenyewe. Watu wa aina hiyo wanao uwezo wa kusaka msaada popote pale wanapoona
panafaa, ila kwa kiasi kikubwa tunao watoto ambao hawana vipaji vya namna hiyo.
Na hakuna wataalamu wa kuwezesha utambuzi wa jambo hilo, walimu wetu
hawaandaliwi kufanya jambo hilo kwa watoto wala wazazi wao.
Lakini ukweli wa jambo hili ni
kwamba, inawezekana kabisa kumtambua mtoto amezaliwa kuwa nani katika maisha
yake yajayo, zipo elimu nyingi za kuwezesha utambuzi wa jambo hilo, kuna elimu
za saikolojia, filosofia, sosholojia, elimu ya unajimu na malezi mbalimbali.
Wazazi ndio wangekuwa wa kwanza sasa kupewa maarifa hayo ili wajue namna
ipasayo kulea watoto wao, elimu hiyo wazazi wanaweza kuipata kupitia viongozi
wao wa dini, kupitia waelimishaji rika, na wafanyao kazi za kutoa ushauri wa
malezi.
Nb: Mada hii itakuwa na
mwendelezo wake kwa kuendelea kujadili suala la elimu kwa mapana yake, ili
wazazi na wadau wa elimu kupata nuru ya kufanya maamuzi sahihi.
By Mkoba Andrian.
0 comments:
Post a Comment