“Kama elimu ni ghali, jaribu
ujinga” sio msemo mgeni huu masikioni mwako, hilo naamini ni jambo lililo wazi
kabisa kwetu sote ya kwamba elimu ni ghali hasa katika maisha ya sasa. Elimu
imekuwa ghali sana kutokana na mabadiliko mbalimbali ya kimaisha duniani kote
na hapa Tanzania pia. Kipindi cha ukoloni na miaka ya mwanzo ya uhuru elimu
ilitolewa bure kwa wananchi kwa kuwa idadi kubwa ya watu ilikuwa haina elimu ya
kimagharibi.
Na pia kulikuwa na idadi ndogo ya
watu hivyo serikali iliweza kumudu kugharamia maisha ya watu wake katika
upatikanaji wa elimu na masuala mengine ya kijamii. Kumbuka katika makala ya
awali nilizungumzia kuhusu aina kuu tatu za elimu, linapokuja suala la elimu
rasmi basi moja kwa moja tunazungumzia elimu yenye asili ya kimagharibi. Hivyo
kwa upatikanaji wa aina hiyo ya elimu tunaingia rasmi katika mfumo wa maisha ya
kimagharibi, kwa hiyo hakuna namna ya kukwepa moja kwa moja gharama ya elimu
kwa kuwa upatikanaji wa elimu hiyo ni wa gharama.
Kwa kuzingatia hilo la gharama ya
upatikanaji wa elimu rasmi, ndipo tuendelee kujadiliana hoja yetu ya msingi
kuhusu namna ya kuelimisha watoto wetu na wa jirani zetu. Katika hili nianze
kusema wazi kabisa watoto wengi huwa wanazaliwa wakiwa safi kabisa katika afya
zao za mwili, roho na akili. Ingawa pia wapo kwa idadi ndogo wale wanaozaliwa
wakiwa na hitilafu. Kila mtoto anapozaliwa huwa amezaliwa kutimiza lengo
maalumu nikiwa na maana ya mtoto wako ndugu msomaji na mtoto wa jirani yako
pia. Hivyo kwa pamoja watoto hao ndio wanaweza kuendeleza gurudumu la maendeleo
yao na ya jamii kwa ujumla wake.
Akili ya mtoto anapozaliwa haina
uhusiano wowote na uwezo wa kiuchumi wa wazazi waliomzaa. Ila kuna uwezekano
mkubwa wa mtoto huyo kuwa na vinasaba vya akili inayofanana na hao wazazi wake
waliomzaa. Kumbuka ule msemo maarufu wa “Mtoto wa nyoka ni nyoka” nao unaweza
kuleta maana katika maelezo yangu hapa kuhusu akili ya mtoto kurandana na ile
ya wazazi wake. Kama mwanazuoni wa kijapani Okumura (2010) alivyoelezea katika
ripoti yake ya utafiti juu ya ushawishi wa wazazi katika tabia za watoto wao.
Ni wazi sasa unaweza kujiuliza
maswali kadhaa ikiwa suala zima la elimu linakuwa hivyo je watu walio maskini
wa kipato na watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanawezaje sasa kupata
tunu ya elimu kama ilivyo kwa watoto wanaozaliwa katika mazingira mazuri ya
kipato? Pamoja na maswali mengine yafuatayo;
·
Jukumu la elimu ni la nani?
·
Watoto wanaoishi katika mazingira magumu ni
jukumu la nani kuwapatia elimu?
·
Jamii inawapokeaje watoto wanaoishi katika
mazingira magumu?
·
Mazingira magumu ni yepi kwa watoto?
·
Nani anasababisha mazingira magumu kwa watoto?
·
Nini wajibu wa serikali kwa watoto wanaoishi
katika mazingira magumu?
Hayo ni miongoni mwa maswali ambayo kama mwana jamii
unaweza kujiuliza na kuona ni kwa namna gani unaweza kuwa mwanaharakati wa
elimu ya watoto wako na wa jirani yako. Ni kweli tunao wajibu wa kubadilisha
namna yetu ya kufikiri kuhusu elimu na maendeleo ya jamii yetu.
Neno mazingira magumu linaweza
kukosa maelezo ya moja kwa moja kumuelewesha mtu mpaka akaelewa, ila kwa faida
ya hoja yangu ya msingi itoshe kusema ni hali ya umaskini wa kipato uliokithiri
unaomkabili mtoto na familia inayomlea. Kwa hapa nchini kwetu Tanzania zipo
kaya ambazo zinaishi kwa pato la chini ya dola moja ya Kimarekani. Ni kawaida
katika Nyanja ya kiuchumi kufanya ulinganifu wa hivyo kuhusiana na kipato cha
kaya moja na nyingine.
Watoto wanaoishi katika
mazingira magumu wana changamoto kubwa katika suala la upatikanaji wa elimu, wanakosa
mambo mengi ya msingi ikiwemo motisha ya wao kupenda maisha ya kujifunza kama
ilivyo kwa watoto wengine wa rika lao. Wanakosa vifaa muhimu vya kuwawezesha
kumudu changamoto za kielimu mfano; sare za shule, viatu, madaftari, kalamu, vile
vile kwa wanaokaa mbali na shule suala la usafiri na upatikanaji wa chakula.
Mwanafalsafa wa kigiriki
anayeheshimika sana duniani katika masuala ya kielimu alipata kunena mtu aliye
na njaa hawezi kumudu kufanya tafakari nzuri. Kwahiyo ni wazi inahitaji mtu
aweze kuwa na amani ya nafsi na mwili wake kwa ujumla ili aweze kumudu suala
zima la kushiriki katika kujifunza. Unapozungumza kuhusu mtoto anayeishi katika
mazingira magumu huwa anapitia maangaiko makubwa sana ya kimaisha ambayo ni
ngumu sana kumpa motisha ya kupenda kufuatilia masomo.
Mazingira magumu ni magumu
hasa, kwani mtoto anapotoka shuleni baada ya kazi kubwa ya kujifunza
aliyoifanya akiwa shuleni, arudipo nyumbani angependa akute mazingira mazuri
yaliyo rafiki. Ikiwemo wazazi ama walezi wenye furaha na amani, akute chakula
cha kumuwezesha kurudisha nguvu yake aliyoipoteza shuleni. Lakini mazingira
hayo ni nadra kwa watoto hao wanaoishi katika mazingira magumu hilo kwa kiasi
kikubwa linachangia watoto hao kuchukua uamuzi wa kuacha shule ili waweze
kupata muda wa kujitafutia pesa za kujikimu ikiwemo na kulea familia zao pia.
Katika jamii zetu wapo watoto
wadogo wanao wajibika kutunza familia zao, bila kujali huo umri wao mdogo. Kaya
maskini kwa hakika zina msukumo mbaya kwa maisha ya watoto wao. Wapo watoto
wanaoingia katika ajira zisizo rasmi ikiwemo wizi na biashara ya ukahaba ili
waweze kupata pesa za kusaidia familia zao.
Ni jambo linalohitaji mkakati
mzuri wa kimaendeleo kwa jamii yetu kuona umuhimu na namna nzuri ya kuweza
kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili kuepushia taifa letu
janga kubwa linaloweza kutokea kwa kuwa na kundi kubwa la vijana lisilo na
elimu stahiki. Ingawa si nia ya hoja yangu lakini si vibaya nikisema tukio
lililotokea la vijana wanaojiita “Panya Road” ni ishara ya jamii iliyokithiri
katika hali duni ya kimaisha. Kwa kuwa kundi kubwa la vijana waliostahili kuwa
shuleni na wengine vyuoni ndio hao wanaoshiriki katika vitendo vya uhalifu.
Bila juhudi ya makusudi
kukabiliana na suala hilo la kuwapatia watoto na vijana wetu elimu, basi
tutarajie mambo kama hayo yakitendeka mara kwa mara. Hivyo kwa namna moja ama
nyingine hata waliopata nafasi ya kusoma hawatakuwa tena na amani ya maisha yao
kwa kuwa wale wasiosoma watahitaji kugawana nao pato lao kwa kutumia nguvu zao
kwa kuwakaba na hata kuwaua.
0 comments:
Post a Comment