Tunaelimishaje watoto wetu na wa jirani
zetu?
‘Elimu ni
ufunguo wa maisha’ ‘ Elimu ni bahari’ ‘Elimu ni mkombozi’ ‘ Kama elimu ni ghali
jaribu ujinga’ hizo ni semi ambazo tunakutana nazo mara kwa mara katika
upashanaji habari na utafutaji habari kwenye maisha yetu ya kila siku.
Elimu ni kitendo
kinachofayika kuhamisha taarifa, maarifa na ujuzi toka kizazi kimoja kwenda
kizazi kingine. Mara nyingi ni kizazi kilichotangulia kwenda kizazi
kinachofuatia lakini pia inawezekana kuwa kinyume chake. Elimu inawezekana kwa
mwongozo wa mtu mmoja kumuongoza mwingine ama mtu kujiongoza mwenyewe katika
kupata elimu husika.
Elimu utolewa kwa namna kuu tatu ambazo ni
namna rasmi, namna rasmi kiasi na namna isiyo rasmi kabisa. Naposema rasmi
namaanisha namna ya utoaji wa elimu kwa utaratibu maalum uliopangwa na mamlaka
za elimu katika nchi. Utaratibu unaweza kuwa umri, mazingira ya kujifunzia,
kipindi cha mafunzo n.k mfano wa mamlaka
za elimu ni Wizara ya elimu yenye jukumu hilo hapa Tanzania. Baada ya kupata
mafunzo yaliyokusudiwa mhitimu anapatiwa cheti cha kuthibitisha elimu aliyopata
kwa utaratibu uliopangwa.
Elimu rasmi
kiasi inatofautiana na nyingine kwa namna ambayo nayo utolewa kwa wanaojifunza,
utaratibu wa elimu isiyo rasmi unatofautiana na utaratibu wa elimu iliyo rasmi
kwa mambo kadhaa ikiwemo umri, mazingira ya kujifunzia, utolewaji wa vyeti kwa
wahitimu na muda wa kujifunza mpaka kuhitimu mafunzo yaliyokusudiwa.
Elimu isiyo
rasmi kabisa, ni ile mtu anaipata kupitia vyanzo mbalimbali katika mazingira
tofauti tofauti na hakuna utaratibu maalum wa kujifunza. Hakuna utaratibu wa
kupatiwa cheti kwa namna hii ya kujifunza kwa vile hakuna mtu anayewajibika kwa
mwingine katika namna ya elimu ipatikanayo. Mfano wa elimu hii ni pale mama
anapomfundisha mwanae kupika na kufanya kazi za usafi nyumbani, baba
anapomfundisha kijana wake kazi ya uvuvi ama kusuka vikapu n.k
Ambacho
tunapaswa kukifahamu ni kwamba, kila mtu anapitia katika namna zote za
upatikanaji wa elimu kwa namna mbalimbali kupitia familia zetu, dini zetu, rika
katika jamii zetu na kupitia jamii nzima ikiwemo mamlaka ya nchi. Pia kwa
kupitia vyombo mbalimbali vya habari huwa tunajifunza masuala mbalimbali katika
jamii zetu.
Tukirejea katika
hoja ya msingi ambayo nimeifanya kama kichwa cha makala yangu, tunaweza sasa
kujiuliza maswali mbalimbali kuhusu elimu, baadhi ya maswali hayo ni kama
ifuatavyo;
·
Lengo la elimu ni nini?
·
Nani anawajibika kwa upatikanaji wa elimu?
·
Elimu gani ifaayo kutolewa kwa kila kundi katika
jamii?
·
Mwenye elimu ana wajibu gani kwake na kwa jamii
yake?
·
Jamii ina wajibu gani kwa mtoa elimu?
·
Mtoa elimu anastahili kuwa na sifa gani?
·
Njia gani ifaayo kutoa elimu?
·
Lugha gani ifaayo kutumika katika utoaji wa
elimu?
Naamini unaweza
kuona hapo maswali ni mengi mno tunayoweza kujiuliza, ni changamoto kubwa iko
mbele yetu kuweza kupata majibu ya maswali haya na mengineyo kuhusu elimu.
Kwa kufahamu
maana ya elimu na namna ya upatikanaji wa elimu tunaweza sasa kuona ya kwamba
elimu ni sehemu ya maisha mwanadamu (mtu). Kwa maana ya kwamba mtu ni mwanaelimu,
kila mtu anazaliwa kwa lengo la kuwa mwanaelimu kuanzia katika ngazi ya familia
na hatimaye jamii kwa ujumla wake.
Ni vema sasa
kuanza kuweka uzito katika jambo la elimu kwa kuwa lengo kuu la uwepo wetu hapa
duniani ni kuwa na elimu ya kutosha (maarifa). Na kwamba sote ni ndugu kwa
maana ya uumbwaji wetu. Tunao wajibu kwa ndugu wote katika ulimwengu wa elimu,
kuhakikisha watoto wetu na watoto wa jirani zetu wanapata elimu stahiki kwa
manufaa ya jamii zetu.
Nb: Mada hii itakuwa na
mwendelezo wake kwa kuendelea kujadili suala la elimu kwa mapana yake, ili
wazazi na wadau wa elimu kupata nuru ya kufanya maamuzi sahihi.
Written by : Mkoba Adrian.
Written by : Mkoba Adrian.
0 comments:
Post a Comment