JE MZAZI UNAYAJUA
MAJUKUMU YAKO KWENYE MAENDELEO YA ELIMU ?
Na Makirita Amani
Miaka ya
hivi karibuni kumekuwa na anguko kubwa sana kwenye maendeleo ya elimu.
Wanafunzi wengi sana wamekuwa wakifeli katika mitihani yao hasa ya kidato cha
nne. Katika kufeli huku lawama nyingi sana zimetolewa kwa watu wanaohusika na
kuporomoka huku kwa elimu.
Tumeona kila mtu akilaumu serikali kwa kutoweka kipaumbele
kwenye maendeleo ya elimu. Serikali imelaumiwa kwa kujenga shule nyingi ambazo
hazina walimu, vitabu au maabara. Na pia serikali imelaumiwa kwa kutojali
maslahi ya walimu na hivyo walimu kufanya kazi kwenye mazingira magumu na hivyo
kuchangia kushuka kwa elimu.
Tumeona pia walimu wakilaumiwa sana kwenye kushuka huku kwa
elimu. Walimu wanalaumiwa kwa kutozingatia majukumu yao na hivyo wanafunzi
kukosa masomo. Na pia walimu wanalaumiwa kwa kuwa na mgomo baridi ambao
unapelekea wanafunzi kukosa usimamizi mzuri shuleni na hivyo kupunguza ufaulu.
Hayo ndio makundi mawili ambayo yamelaumiwa sana kwenye
kushuka kwa elimu yetu. Je hawa tu ndio wanaostahili lawama? Je upi ni mchango
wa wazazi katika kukua na kuporomoka kwa elimu yetu? Ukweli ni kwamba wazazi
wana nafasi kubwa sana katika kukua au kuporomoka kwa elimu. Kwa wanafunzi
wanaosoma shule za kutwa, wanatumia muda mwingi nyumbani kuliko wanaotumia
shuleni. Hii ina maana kwamba kama wazazi wangekuwa makini na maendeleo ya
watoto wao shuleni wangekuwa watu wa kwanza kufuatilia kama watoto hawafanyi
vizuri. Lakini hiki sio kinachotokea. Wazazi wamesahau kabisa majukumu yao na
kuona walimu ndio wenye majukumu yote kuhusiana na elimu.
Ugumu wa maisha umewafanya wazazi kufanya kazi kwa muda
mrefu na hivyo kukosa muda wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni.
Wazazi wanaamini kwamba kwa kulipa ada shuleni ndio wamekamilisha wajibu wao
kwenye elimu. Hii sio sahihi kabisa.
Yafuatayo ni majukumu
ya kila mzazi katika maendeleo ya elimu ya mtoto
1. Mzazi
anatakiwa kujua vipaji vya mtoto wake. Mzazi ndio anakuwa karibu sana na mtoto
hata kabla hajaenda shuleni. Kwa kuwa nae karibu anaweza kuona ni vitu gani
mtoto anapendelea na hivyo kufanya. Kwa kujua vipaji vya mtoto kutamfanya mzazi
aweze kuashauriana na walimu jinsi ya kuweza kuendeleza vipaji vya mtoto wake.
2. Mzazi
anatakiwa kujua maendeleo ya kila siku ya mtoto wake shuleni. Mzazi usisubiri
ripoti ya nusu mwaka au ya mwaka kujua mtoto wako amekuwa wa ngapi darasani.
Unatakiwa kufuatilia maendeleo ya mtoto wako kila siku. Jua ni kazi gani
amepewa za kufanya nyumbani na hakikisha amezifanya kwa usahihi. Pia mzazi
anatakiwa kujua maendeleo ya mtoto wake kinidhamu, maana bila nidhamu mtoto
hawezi kufaulu vizuri.
3. Mzazi
anatakiwa kujua changamoto ambazo mtoto anazipitia shuleni. Inawezekana mtoto
anaonewa na wanafunzi wenzake ila anaogopa kumwambia mwalimu kwa sababu
ataonewa zaidi. Wewe kama mzazi ukiwa na urafiki na mtoto wako itakuwa rahisi
kuona pale ambapo anapitia changamoto mbalimbali. Kwa kujua hivyo unaweza
kuangalia njia nzuri inayoweza kumsaidia mtoto wako ili aweze kuwa na mazingira
mazuri shuleni.
4. Mazazi
anatakiwa kumjengea mtoto wake mapenzi mazuri na elimu ili mtoto awe na mtizamo
mzuri kuhusu elimu. Mzazi anatakiwa amweleze mtoto kwa nini ni muhimu kwake
yeye kusoma na kufaulu vizuri. Pia ampe moyo pale ambapo anashindwa na
kumhamasisha kuweka juhudi zaidi kwenye masomo yake.
5. Mzazi
anatakiwa kumfundisha mtoto mambo ambayo hapati nafasi ya kufundishwa shuleni.
Sio mambo yote muhimu kwenye maisha mtoto anafundishwa shuleni, kama mzazi
atapata nafasi ya kukaa na mtoto wake anaweza kumfundisha mambo ya ziada ambayo
yatamsaidia shuleni na hata kwenye maisha.
Tatizo ni kwamba wazazi wengi nchini hasa wanaoishi katika mazingira magumu hawajui majukumu yako. Na inamfanya mzazi ajue kulipa ada na kununua mahitaji mengine ya shule kwa mtoto ndio wajibu wake na akifanya hivyo basi hana majukumu mengine katika maendeleo ya mtoto wake. Kwahiyo ni bora zaidi kama serikali na wadau mbalimbali wa elimu watawasaidia wazazi kujua majukumu yako katika maendeleo ya elimu
ReplyDelete